Wafanyakazi Watapata Ruhusa ya Kushiriki Katika Uchaguzi Mkuu
Dar es Salaam – Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imezitaka taasisi zilizo chini yake kutoa ruhusa kwa wafanyakazi waliojiandikisha nje ya vituo vyao vya kazi ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Tamko hili limefanywa wakati zimebaki siku mbili tu kabla Watanzania kwenda kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani watakawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkurugenzi wa Usimamizi Mashirika ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amesema hayo leo Oktoba 27, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mauki amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watumishi wote wa umma waliopo katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini wanatumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu.
"Kupiga kura ni jambo la mabadiliko chanya, yanayowawezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji. Ushiriki mkubwa wa watumishi wa umma unaonesha mfano wa uzalendo, nidhamu ya kitaifa na uelewa wa majukumu ya kikatiba," amesema Mauki.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina inaamini kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu, watumishi wa umma wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha utawala bora, uchumi endelevu na ustawi wa wananchi.
Ili kufanikisha hilo, OMH imewataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha watumishi wao wanapatiwa fursa ya kutekeleza haki hiyo muhimu bila kuathiri majukumu yao ya kikazi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Mauki ameeleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au masilahi.
Mwito huu unakuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan tayari ametangaza Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika shughuli muhimu ya kupiga kura.