Polisi Kagera Wadharau Amri ya Mahakama ya Kuwaachia Watuhumiwa
Oktoba 23, 2025, Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Bukoba, kupitia maombi maalumu (Habeas Corpus), ilitoa amri kwa Jeshi la Polisi kuwaachia huru au kuwafikisha kortini, watuhumiwa wa uhalifu wanaowashikilia kinyume cha sheria.
Lakini badala ya kutekeleza amri hiyo ya mahakama, TNC imepata taarifa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, amejitetea kuwa hawajapokea amri hiyo ya mahakama na kwamba sio kazi yao kuwafikisha kortini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Kamanda huyo amesema kazi yao ni kukamata na kupeleleza kisha kuandaa jalada na kulipeleka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), ambao ndio wana wajibu wa kupima kama kuna viashiria vya jinai na kuandaa mashitaka.
Hali ya Kutatanisha katika Utekelezaji wa Sheria
Msimamo huo wa Polisi umesababisha wasiwasi mkubwa hasa kwa kuwa waliwakilishwa kortini na wakili mwandamizi wa Serikali, Judith Mwakyusa akisaidiana na mawakili, Mgeni Mdee na Matilda Assey, hivyo walifahamu amri ya mahakama ilisema nini.
Katika maombi hayo mawili tofauti namba 25115 na 25281 ya 2025, wajibu maombi walikuwa ni Mkuu wa Kituo (OCS) Bukoba, Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Kagera na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) Kagera.
Waleta maombi walimuunganisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kama mjibu maombi wa nne na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kama mjibu maombi wanne, ambaye ndiye mwenye wajibu wa kuandaa hati ya mashitaka.
Viongozi wa Chadema Washikiliwa Kinyume na Sheria
Msingi wa maombi hayo unatokana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huko Bukoba na raia wengine wawili, ambao wanashikiliwa mahabusu kwa zaidi ya siku nane nje ya saa 24 zinazotajwa na sheria.
Mahakama baada ya kupima hoja za pande mbili, ilitoa amri ama watuhumiwa hao waachiwe huru au wawafikishe mahakamani si zaidi ya Oktoba 24, 2025. Hawajawafikisha kama amri ya mahakama ilivyowataka.
Badala ya kutekeleza amri hiyo ya mahakama, Oktoba 25, 2025 RPC Kagera alijitokeza na kutoa visingizio mbalimbali licha ya kuwa kuna utaratibu wa kupinga amri za mahakama.
Kudharau Mahakama ni Kosa la Jinai
Kitendo kinachofanywa na Polisi cha kutotekeleza amri ya mahakama ni kuudharau mhimili huo kama inavyofafanuliwa na kifungu cha 114A cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Kifungu cha 114A (b) kinasema mtu anatenda kose endapo kwa makusudi ana kinga, au kwa kujua anazuia, au kwa kuingilia au kuzuia utekelezaji wa hati yoyote ya kuitwa shaurini, notisi au amri iliyotolewa na mahakama.
Endapo ataitwa kortini (show cause) ili kujieleza na akaonekana amekiuka amri hiyo ya mahakama au maelekezo yoyote, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha muda usiozidi mwaka mmoja.
Kwa hiyo wajibu maombi wako katika hatari ya kufungwa jela kwa kukiuka amri ya mahakama.
Utawala wa Sheria Lazima Uzingatiwe
Nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria. Kwa lugha ya kawaida kabisa, maana yake hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia Rais wa nchi mpaka raia wa kawaida na kuanzia Dola ya nchi mpaka kaya iliyopo kwenye kijiji kidogo kabisa.
Kila chombo cha Dola, taasisi, kila mtu anawajibika kwa sheria wakiwamo Jeshi la Polisi.
Dhana kwamba ni vema watu watawaliwe na sheria imeanza zamani za kale. Hammurabi, Mfalme wa Babylon, alitengeneza sheria na kuzipa uzito mkubwa, hii ilikuwa miaka 1760 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, zaidi ya miaka 3,785 iliyopita.
Aristotle, aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, alitamka kuwa "Utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi".
Hatari ya Kutumia Vibaya Madaraka
Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizaji ambayo hutokea pale utawala wa sheria haupo.
Ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi ya raia. Kwa hiyo Utawala wa sheria unapaswa kuanzia kwa watawala bila kuwepo kwa visingizio visivyo na mashiko.
Hayati Lord Denning (1899-1999) ambaye alikuwa Jaji maarufu wa Uingereza alisema; "Pale ambapo madaraka makubwa yanatolewa kwa vyombo vya Dola basi ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya."
Polisi Wanatakiwa Kufuata Sheria
Sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai (CPA), inataka mshukiwa wa uhalifu aliye mikononi mwa Polisi afikishwe kortini ndani ya saa 24. Hakuna sababu ya Polisi kuwa juu ya sheria na kudharau amri za mahakama.
Mwaka 1765 Lord Camden ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Uingereza alisema: "Iwapo ni sheria, basi tutaiona kwenye vitabu vyetu vya sheria. Iwapo haipo humo, basi hiyo sio sheria."
Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.
Chuki dhidi ya Askari Inaongezeka
Leo hii nchini kwetu chuki dhidi ya askari wetu ni kubwa mno na ukitafuta kiini ni wao kukiuka sheria katika ukamataji na upelelezi na kuweka watu mahabusu siku zozote wanazotaka kinyume kabisa na sheria na Katiba ya nchi.
Hakuna mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria au nje ya sheria. Kila mmoja wetu anawajibika kwa sheria.
Lord Templeman alisema; "Bunge linatunga sheria, serikali inatekeleza sheria, na mahakama zinathibitisha sheria."
Vyombo vyote hivi vya Dola vinalazimika kufanya kazi yake ndani na chini ya sheria ili kulinda haki za wananchi ambao mara nyingi huitwa "wanyonge" na havipaswi kufanya kazi kwa masilahi ya kisiasa ya kundi fulani, bali kwa mujibu wa sheria.
Siku zote kunapofuka moshi chini huwa kuna moto. Ni muhimu kurudi kwenye msitari kabla haijachelewa.