Jinsi ya Kuona Tena Video Zilizopotea kwenye Instagram
Dar es Salaam – Watumiaji wa Instagram wanapaswa kufahamu wanaweza kuiona tena ile video ambayo wameipenda ila kwa bahati mbaya imepotea aidha kwa kuji-refresh au kutoka kabisa kwenye timeline ya mtandao huo.
Mfano unaangalia video kisha ukaipenda ila kabla hujaipakua au kushea kwa mwenzio ikapotea na hujui utaipata wapi basi unapaswa kufanya yafuatayo ili kuiona tena.
Kwa sasa mtandao huo wenye watumiaji zaidi ya bilioni mbili kila mwezi na takribani milioni 500 kila siku umekuja na kipengele kipya cha kuiona tena post iliyokupotea.
Ikumbukwe Instagram ni jukwaa la mtandao wa kijamii lililozinduliwa mwaka wa 2010 sasa linamilikiwa na Meta Platforms, Inc., kampuni mama ya Facebook na imekua ikija na masasisho kila wakati ili kuboresha huduma zake.
Hatua za Kuona Tena Video Zilizopotea
Ili kuiona tena video hiyo unatakiwa kwenda kwenye kipengele cha Setting, kisha nenda palipoandikwa ‘Your activity’ shuka chini kisha utaona mahali pameandikwa ‘Watch History’.
Ukifungua watch history utaona video zote ambazo umeziangalia ikiwa ni kwa muda wa siku 30. Hivyo ambayo ilikupotea utaiona hapo.
Vilevile ukiwa katika kipengele hichohicho cha ‘Your activity’ unaweza kuangalia post zote ulizo ‘likes’, comments au reposts, tag.
Katika kipengele hicho cha ‘your activity’ unaweza kuangalia historia yako ya kutafuta vitu kwa kwenda kwenye kipengele cha ‘recent searches’ kisha ukaangalia akaunti ulizotafuta.
Udhibiti wa Muda wa Matumizi
Unaweza kuweka muda wa kuperuzi kama unatumia muda mwingi.
Pia, unaweza kuangalia muda unaotumia kuperuzi kwenye Instagram kwa muda wa juma zima kwa kwenda chini utakuta kipengele kimeandikwa ‘Time spent’ kisha utaona kwa kuanzia Jumatatu umetumia saa ngapi kuperuzi hadi Ijumaa.
Ukiona unatumia muda mrefu kwa siku na unataka kujizuia unaweza kuweka kikomo kwa kushuka chini utakuta sehemu imeandikwa daily limit kisha unachagua utumie Instagram kwa dakika 15 kwa siku, 30, 45, saa moja au mawili.
Ukishaweka muda basi Instagram watakutumia ujumbe wa kufunga mtandao huo wakati unatumia na muda umeshafika.