Mwanaume Atoa Ushauri kwa Mwenziwe Anayeombwa Kuendeleza Mahusiano na Mpenzi wa Zamani
Mwanaume mmoja ametoa ushauri muhimu kwa mwenziwe anayekabiliwa na changamoto ya mpenzi wake wa zamani kuomba kuendeleza uhusiano wao licha ya wote kuwa wameoa.
Katika hali hiyo, mwanaume huyo alikuwa na uhusiano wa mapenzi na binti mmoja kwa miaka kadhaa kabla ya kuachana na kila mmoja kushika njia yake.
Baadaye yeye alioa na amebahatika kupata watoto wawili, mwenzake pia alikuwa ameolewa na ana mtoto mmoja.
Jambo la ajabu ambalo linaweka mzunguko ni mpenzi wake wa zamani kumganda kuendeleze uhusiano wao akidai wakati huu wamekuwa kiakili na watafurahia sana kuliko wakati ule maisha yalikuwa yakiwasukuma huku na kule.
Licha ya ukweli kuwa huyu mwanamke alimpenda sana, wazo lake hili linaumiza kichwa ukizingatia mke wa mtu ni sumu na heshima ya ndoa ni muhimu.
Ushauri wa Wataalamu
Wataalamu wanashauri kwanza hongera kwa uamuzi wa kuheshimu ndoa na kutambua kwamba mke wa mtu ni sumu. Huo ni ukomavu wa kipekee, hasa katika dunia ya leo ambapo maadili ya ndoa mara nyingi yanatetereka.
Jambo hili ni zito kihisia hasa ukizingatia huyu mwanamke aliwahi kuwa mpenzi na walipendana. Muhimu kutambua kuwa anachokifanya huyo mwanamke kukung’ang’ania ni jaribu kama majaribu mengine na inapaswa kulishindwa.
Hisia zilizokuwepo awali hazitakuwa na nafasi tena. Mtu anaweza kuvutiwa lakini kwa muda tu.
Heshima ya Ndoa ni Muhimu
Ndoa ni agano takatifu na jukumu la kimaadili na kiroho. Kwa hiyo, kulinda mapenzi ya sasa ni wajibu wa kwanza kitamaduni, kisheria na kidini.
Kama mwanamke huyo anaendelea kumlazimisha, jambo la kwanza ni kuhakikisha kunakuwa na mipaka baina yao, kutokubali kukaa naye faragha kwa namna yoyote ile.
Pia kutoingia kwenye mkenge wa kujibu ujumbe wake wa mapenzi na kuepuka mawasiliano yasiyo ya lazima. Akiuliza kuhusu masuala tofauti hasa yale muhimu kama ya kazi, kijamii na kiuchumi, mjibu tofauti na hapo kukaa kimya.
Unapokuwa thabiti kwenye msimamo, ataona kwamba hakuna udhaifu wa kihisia anaweza kuutumia kutimiza azma yake hiyo mbaya.
Tahadhari za Kukubali Vishawishi
Heshima ya ndoa ndiyo heshima ya kibinafsi. Wengi wameshuhudia maisha yao yakiharibika kwa kukubali tamaa ya muda mfupi.
Kuiruhusu mwanamke huyo kuingia tena kwenye maisha ya kimapenzi, hautakuwa tu unamsaliti mke bali pia unajiweka katika hatari ya aibu, migogoro, na majeraha makubwa ya kihisia kwa familia zote mbili.
Zingatia kumuomba Mungu akuepushe na vishawishi. Maombi yana nguvu ya kulinda na kuimarisha. Kila unapotaka kudhoofika, jiulize: "Je, ni faida gani nitakayopata nikiharibu amani ya ndoa yangu kwa sababu ya kumbukumbu za zamani?"
Msimamo Thabiti ni Lazima
Usiogope kusema hapana kwani huyo mwanamke siyo tu atakuvunjia heshima yake bali pia atakuweka kwenye migogoro na mumwe. Wahenga walisema: ‘penzi kikohozi kulificha huliwezi’, naamini hata mjifiche vipi mtabainika na mumewe hatokuelewa utajishushia heshima na kutengeneza adui wa kujitakia.
Mwanamke anayejiheshimu humheshimu mumewe na familia yake kwa ujumla. Anachotaka kukifanya si miongoni mwa tabia za wake wema. Ukiweza mweleze wazi kuwa huna mpango wa kuwa na uhusiano naye tena, atulie kwenye ndoa yake.