Baraza la Biashara Afrika Mashariki Lazindua Dawati la Kidijitali la Utoaji Taarifa
Arusha – Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC) limezindua dawati la kidijitali la utoaji taarifa lengo lake ni kusaidia wafanyabiashara wadogo wa mpakani kukabiliana na vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs).
Uzinduzi huu ulifanyika katika mpaka wa Taveta-Holili, ukiambatana na mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara katika elimu ya fedha, usimamizi wa biashara na mbinu jumuishi za kijinsia.
Mradi huu unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana wafanyabiashara wa kilimo cha chakula na kuboresha biashara ya mazao muhimu kama mahindi, mchele, maharage, na mazao ya bustani ndani ya jumuiya.
Lengo kuu ni kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara kwa:
– Kuondoa vikwazo visivyo ya kiforodha
– Kuongeza uelewa wa vyombo vya urahisishaji biashara
– Kuanzisha madawati ya kidijitali ya taarifa za biashara mipakani
Mradi unaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu (2025–2027) unalenga kuwawezesha wafanyabiashara zaidi ya 2,440 katika maeneo ya mpaka.
Naibu Mkurugenzi wa Uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameihimiza jumuiya kuelewa umuhimu wa kuondoa vikwazo vya biashara, kuimarisha miundombinu, na kuhakikisha wanawake na vijana wananufaika kikamilifu.
“Kuwawezesha wafanyabiashara wadogo si tu kuongeza biashara, bali ni kubadili maisha na kuijenga jumuiya endelevu,” alisema.
Mshiriki wa mafunzo, Ester Mbaruku ameipongeza mpango huu, akisema utasaidia wafanyabiashara wadogo kupata ufumbuzi wa haraka wa changamoto zao za biashara.