Dar es Salaam – Mfanyabiashara na kiongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz, amepongeza mchakato mpya wa chama katika uteuzi wa wagombea wa ubunge, akizitaja sifa za haki na uwazi.
Akizungumza katika mahojiano ya leo, Jumapili Agosti 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Rostam alizungumza kuhusu uzoefu wake wa miaka 18 katika michakato ya chama, akitaja nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uanachama wa Halmashauri Kuu, kamati kuu na nafasi ya Mweka Hazina wa Taifa.
“Mchakato huu sasa unaruhusu watiania kujaza fomu, kufanyiwa tathmini ya kina na kisha kurudishwa kwa wananchi kupigiwa kura. Mgombea mshindi wa kura ndiye atakayewakilisha chama, ila tu asipotoa sababu ya kushtusha,” alisema Rostam.
Ameendelea kusisitiza kwamba utaratibu huu mpya ni muhimu sana kwa kuwa unajenga imani ya wanachama na umma kwa chama cha CCM, ukiwa ni mwendelezo wa maboresho ya kidemokrasia ndani ya chama.