Rais Samia Awaomba Waganga Kuepuka Ramli Chonganishi Kabla ya Uchaguzi wa 2025
Mwanza – Rais Samia Suluhu Hassan amewasihi viongozi wa kimila, hususani waganga wa kienyeji, kujiepusha na ramli chonganishi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili kuhakikisha amani.
Akizungumza kwenye tamasha la kiutamaduni la Bulabo wilayani Magu, mkoani Mwanza, Rais alisema kipindi hiki waganga watatembelea na watu mbalimbali wanaotaka kugombea nafasi za uongozi.
“Ombi langu kwa ndugu zetu wa kimila… waganga wa kienyeji, kipindi hiki wanaoomba kupata nafasi mbalimbali watawatembelea. Niwaombe wasifanye ramli chonganishi kwa sababu hizo ndizo zinaweza kuvunja amani kwenye uchaguzi,” alisema.
Rais alishauri mgombea atakayeingia katika uchaguzi awe na tabia nzuri, asambaze amani na usichokoe chuki. “Kama unakuja, enda vizuri, kula pesa yako nenda kalale. Twende tufanye mambo kwa murua ili watu wote waende vizuri na tumalize uchaguzi vizuri.”
Amewaomba machifu na watemi kudumisha mila na desturi za Kitanzania, akizitaja kama kielelezo cha uhai wa jamii. Alisema utamaduni ni muhimu sana katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika ulimwengu wa kisasa.
“Utamaduni hubeba na kurithisha imani, tabia na maadili yanayofaa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine,” alisema Rais, akiwataka viongozi wa kimila kuendelea kulinda na kurithisha tamaduni njema kwa vizazi vijavyo.
Tamasha la Bulabo lilitoa fursa ya kurithisha, kuhifadhi na kuendeleza mila za Kitanzania, ambazo ni msingi wa utambulisho wa Taifa.
Wakati wa sherehe, machifu wa nchi nzima walimkabidhi Rais Samia kiti cha kichifu kwa awamu ya pili, kumtambulisha kama Chifu Hangaya kwa miaka mitano.
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 unatarajiwa kuwa ya amani na ya kidemokrasia, na Rais Samia amewataka wananchi kushiriki kikamilifu.