WAOGELEAJI 14 WAANDAA TIMU YA TAIFA KWA MASHINDANO YA VIJANA YA AFRIKA
JUMLA ya waogeleaji 14 wameunda timu ya Taifa kujiandaa na mashindano ya vijana ya kuogelea ya Afrika yatakayofanyika kuanzia April 30, hadi Mei 3, mwaka huu nchini Misri.
Msemaji wa Chama cha Kuogelea Tanzania alisema kuwa timu hiyo imeshaanza maandalizi ya michuano hiyo kuhakikisha inakwenda kushiriki na kufanya vizuri.
“Kati ya waogeleaji hao, saba ni wanaume na wengine saba ni wanawake. Uchaguzi wa kikosi umetokana na mashindano mbalimbali yaliyopita ikiwemo iliyofanyika wiki mbili zilizopita,” alisema.
Timu ya waogeleaji inajumuisha wanaume saba: Romeo Mwaipasi, Aryan Bhatt, Mark Tibazarwa, Austin Okore, Christian Fernandes, Enrico Baretto, na Sahal Haarunani.
Wanawake watakaoshiriki ni Filbertha Demello, Lina Goyayi, Bridget Heep, Natalia Ladha, Amylia Chali, Aliyana Kachra na Aminaz Kachra.
Mashindano haya yataibua fursa muhimu kwa waogeleaji vijana wa Tanzania kuonyesha vipaji vyao kwenye kiwango cha kimataifa.