Serikali Yazielekeza Taasisi Kusaidia Wajasiriamali Kukua na Kuwa Shindani
Serikali imezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasaidia wajasiriamali kukua na kuendelea kuwa shindani ili waweze kuzalisha kwa tija na kuuza kwenye masoko ya ndani na nje.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara amesema hatua hii itaongeza ajira kwa vijana na wanawake, kupata fedha za kigeni na kupunguza uingizwaji wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa nchini.
“Maelekezo ya Rais ni kwamba sekta binafsi iwe kiongozi katika kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati, daraja la juu, jumuishi na viwanda. Wajasiriamali ndio wanaozalisha bidhaa mbalimbali ambazo zinakwenda kwa walaji na viwanda vya juu,” alisema.
Ametoa mifano ya bidhaa kama mafuta ya kula, sabuni na zinginezo ambazo sasa zinazalishwa ndani ya nchi badala ya kuingizwa.
“Tunataka fedha zetu zitumike kununua bidhaa ambayo hatuwezi kuzalisha. Tupende bidhaa zetu za ndani, tutakuza uchumi, wajasiriamali na tuondokane na dhana ya vijana wasio na ajira,” alisema.
Naibu Waziri ameahidi kuwa serikali itasaidia wajasiriamali wanawake na vijana kufikia malengo yao na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.