WAZIRI MKUU MAJALIWA AITAKA VIONGOZI WA DINI KUPAMBANA NA MMOMONYOKO WA MAADILI
Arusha – Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito muhimu kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kukemea vitendo vinavyochangia mmomonyoko wa maadili, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza wakati wa Siku ya Maridhiano Kitaifa, Majaliwa amesisitiza kuwa changamoto zinazokumba taifa ni pamoja na mabadiliko ya teknolojia na ushawishi wa tabia za Magharibi, ambazo zinachangia uharibifu wa maadili.
“Mfano wa bangi hapa Arusha haifai kabisa. Tunataka kupunguza na kuondoa kabisa matumizi ya dawa za kulevya. Tumezuia dawa kuingizwa kupitia vituo mbalimbala na njia zisizo rasmi,” alisema Majaliwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, alisema kuwa ni muhimu kuondoa chuki katika jamii na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
Majaliwa amesisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu ya kutoa miongozo kwa jamii, hasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, na waendelee kushirikiana na Serikali ili kudumisha amani na mshikamano.
Waziri Mkuu amewasihi viongozi wa dini kuwa walinzi wa maadili ya jamii, kuelekea uchaguzi ujao.