Ripoti Mpya Yathibitisha Umuhimu wa Michango ya Diaspora Kiuchumi
Dar es Salaam – Benki Kuu ya Tanzania sasa imezindua ripoti muhimu inayofuatilia michango ya fedha kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, jambo ambalo litakuwa muhimu sana katika kuboresha uchumi wa taifa.
Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, ameeleza kuwa fedha za Diaspora zina uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya nchi. “Fedha hizi zinaweza kusaidia kufadhili miradi ya muda mrefu, kubadilishana teknolojia, kuboresha mapato ya familia na kusaidia maendeleo ya jamii,” alisema.
Ripoti hiyo imeangazia jinsi fedha za Diaspora zinavyoweza kunufaisha Tanzania, hasa katika kuboresha sekta za afya, elimu, na kuondoa umaskini. Serikali imeshapanga mikakati ya kurahisisha njia za kutuma fedha, ikijumuisha kuanzisha mifumo ya malipo ya kielektroniki.
Uchunguzi unaonesha kuwa kwa nchi kadhaa Afrika, michango ya Diaspora imekuwa kubwa zaidi kuliko misaada ya kimataifa. Kwa mfano, nchini Nigeria, fedha za Diaspora zilifika bilioni 25 mwaka 2022, ambazo zilikuwa sawa na asilimia 6.1 ya Pato la Taifa.
Mtaalamu wa uchumi anasema kuwa umuhimu wa fedha hizi unazidi kukuwa, hususan kwa kuboresha uchumi wa nchi zinazoendelea.