Serikali Imejiandaa Kukuza Uchumi Kwa Kutumia Rasilimali Zilivyopo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inajiimarisha katika kukuza uchumi wake kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuweza kumudu kutekeleza maeneo yote muhimu yakiwemo ya sekta ya afya, elimu na maji.
Wakati wa kipindi cha maswali Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu alisema Tanzania ina uwezo na rasilimali za kutosha kushirikiana na kujenga uchumi wa ndani.
“Uwezo tunao, tunazo maliasili, tunazo rasilimali, kazi ambayo tunayo ni Watanzania kushirikiana kuhakikisha tunatumia maliasili na rasilimali tulizonazo kujenga uchumi wa ndani kuwezesha mipango na bajeti iweze kutekeleza haya,” alisema.
Amethibitisha kuwa nchi inaheshimu sera za mambo ya nje na inatekeleza mikataba kwa mujibu wa sera hizo. Aidha, alipongeza Rais kwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya kimataifa.