AJALI YA GARI NDANI YA HIFADHI YA NGORONGORO: MTALII MMOJA AFARIKI, WENGINE WAJERUHIWA
Arusha – Ajali ya gari iliyotokea ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro jana Jumamosi imesababisha kifo cha mtalii mmoja wa kigeni na kujeruhia wengine watano.
Taarifa rasmi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatangaza kuwa ajali hiyo ilitokea saa 8:45 mchana kati ya viewpoint na lango la Loduare. Gari la utalii lilikuwa na watu saba, sita wakiwa raia wa Israel na mmoja Mtanzania dereva.
Majeruhi walipelekwa mara moja kwenye hospitali za Lutherani na Fame zilizopo wilayani Karatu, na baadaye kusafirishwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center kwa matibabu zaidi.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewataka madereva wote wa magari ya utalii kuzingatia sheria za barabarani na usalama ili kulinda maisha ya wageni.
Uchunguzi kuhusu sababu za ajali unaendelea.