Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepanga kuongeza bajeti ya elimu kutoka Sh864 bilioni hadi Sh1 trilioni, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuongeza ubora wa elimu na kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo nchini.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ametangaza hatua hiyo leo, Desemba 5, 2025, wakati akifungua mkutano mkuu wa 13 wa Jumuiya ya walimu wakuu wa shule za sekondari Zanzibar (Juwaseza), uliofanyika sambamba na uzinduzi wa bweni jipya la wasichana katika shule ya Fidel Castro, Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk Mwinyi alisema ongezeko hilo la bajeti linalenga kuboresha mazingira ya ufundishaji, kuimarisha masilahi ya walimu, kupanua miundombinu ya elimu na kujenga mabweni katika kila wilaya ya Unguja na Pemba.
"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inalenga kuongeza bajeti ya sekta kutoka Sh864 bilioni hadi kufikia Sh1 trilioni ili kuimarisha ubora wa elimu kwa vizazi vyetu," alisema Dk Mwinyi.
Amesema ujenzi wa mabweni au dakhalia kama yanavyofahamika Zanzibar, ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, idadi ya wanafunzi wanaosoma katika shule za bweni inafikia 10,000, hatua ambayo itasaidia kuboresha nidhamu, ufaulu na usawa wa elimu.
Akiwahutubia walimu wakuu, Dk Mwinyi alisisitiza wajibu wao katika kusimamia miundombinu ya shule, kuimarisha ufaulu wa wanafunzi, na kulinda rasilimali za umma.
Aidha, aliahidi kutenga fedha maalumu kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu pindi inapohitajika.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi aliahidi kuyapitia upya masilahi ya walimu wastaafu na watumishi wengine wa umma, ikiwemo kuongeza posho, kuboresha makazi ya watumishi na kuboresha mifumo ya pensheni ili kuinua ustawi wa walimu.
Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdallah Said, alisema ujenzi wa bweni la wasichana kwenye shule ya Fidel Castro umegharimu Sh1.5 bilioni, ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 288, ikiwa ni wastani wa wanafunzi 28 kwa kila darasa.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, wizara inatarajia kujenga mabweni mengine 16 katika mikoa ya Unguja na Pemba, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupanua miundombinu ya elimu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa amesema mageuzi yanayoendelea kushuhudiwa kwenye sekta ya elimu yanatokana na maono, dhamira na juhudi kubwa za Rais Mwinyi katika kuipa sekta hiyo nafasi ya kipaumbele.