Unguja – Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji ametoa ahadi ya kutunza siri za serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ili kulinda maadili ya utumishi wa umma huku akisisitiza umuhimu wa kuvunja makundi.
Meya huyo ametoa tamko hilo Desemba 4, 2025 katika hafla ya kuapishwa kwa madiwani wateule pamoja na uchaguzi wake kuwa Meya na Naibu wake katika Ofisi za Baraza la Jiji Michenzani Unguja.
Haji amesema si jambo la kujivunia kwa mtendaji kusambaza au kuzungumzia taarifa ambazo zipo katika mazingira ya kikazi bila kuzingatia taratibu za serikali.
Amewaagiza watendaji wa baraza hilo kuhakikisha vikao vyao vinakuwa vya siri na kushuka kwa wananchi kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa haraka.
"Nahitiji tufanye kazi kwa ushirikiano na kuvunja makundi kwani hayawezi kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu," amesema Haji.
Meya wa zamani wa Jiji hilo, Mahmoud Mohammed Mussa amesema ni jambo la msingi viongozi hao kuona umuhimu wa kuwa na ustahamilivu na uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.
Ameongeza kwamba kiongozi mwenye dhamana anapaswa kuwa makini kwa kauli na matendo yake ili kulinda heshima ya ofisi pamoja na maslahi ya wananchi.
"Kiongozi anapokula kiapo tayari ametoa uhalali wa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa atakiuka maagizo yote aliyopewa hivyo kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria," amesema Mussa.
Naibu Meya, Haitham Muhidini Khamis amewapongeza wajumbe kwa kumchagua kwa kura za ndio na kuwaomba kushirikiana kwa upendo ili kufanya kazi kwa ufanisi kwani bila ushirikiano hawawezi kufikia lengo lililokusudiwa na serikali.
Hakimu Mkoa wa Mjini, Mummin Ali Juma ameonyesha imani yake kwa viongozi hao akisema bila shaka watatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria na watambue kuwa kiapo hicho wamejikubalisha na kutoa uhalali wa kuchukuliwa hatua wakati wowote endapo watakwenda kinyume.