Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho, kutokuwa wanyonge bali kujibu mashambulizi ya upotoshwaji unaofanywa mtandaoni dhidi ya Serikali.
Amewataka Wana CCM kujibu mapigo hayo, kwa kuwaelimisha Watanzania lakini si kwa kuwatukana watu hao wanaofanya uchochezi, upotoshaji na kubeza jitihada za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali.
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 6, 2025 katika kikao kazi na wanachama na viongozi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam. Vilevile, alitumia kikao hicho kujitambulisha kama mlezi wa CCM wa mkoa huo.
Amewataka viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya mashina, tawi, kata, wilaya na mkoa kwenda katika mitandao kutoa elimu kuhusu upotoshwaji na kuwaeleza wananchi ukweli wa hali halisi iliyopo, ili kuondoa uongo wanaolishwa Watanzania.
"Mwanzoni wakati naanza kuzungumza, niliwaambia kila mmoja wenu awashe tochi katika simu yake, mkawasha. Maana yake kila mtu ana ‘simu janja’, hivi kwa wingi wetu huu tukiamua kuingia kwenye mitandao, kuna mtu atatushinda?" swali lililojibiwa kuwa hakuna.
"Maana yake Wana-CCM tumeamua ku ‘relax’ na tumeacha kutimiza wajibu. Kulinda chama ni wajibu wa kila mwanachama, sisi tuna Serikali, wenzetu hawana Serikali, wanataka watupokonye, lazima tuilinde Serikali yetu. Amani lazima tuilinde, twendeni tukaidhibiti mitandao," amesema.
Kihongosi amesema kuna watu mtandaoni kazi yao kubwa ni kuandika uchochezi, upotoshaji na kuhamasisha vurugu kuanzia asubuhi hadi jioni, akidai kundi hilo lina lengo la kuchafua nchi, kwa sababu kuna watu wapo nyuma yao wanawalipa.
Amesema ifike wakati lazima watu aliowaita wachochezi wa mtandaoni wapingwe hadharani, akieleza zisipofanyika jitihada hizo, Taifa linakwenda kuharibika.
Mbali ya hayo, amesema kuna wengine wapo nje ya nchi wanahamasisha wananchi kuingia barabarani na kufanya vurugu.
"Watu wanajazwa mambo ya ajabu mtandaoni na kila anayejitokeza kupaza sauti ya kukemea mambo maovu anaitwa ‘chawa’ au anajipendekeza, msiogope. Jipendekeze kuilinda nchi yako, amani yako ndiyo usalama wako, hatuna sababu ya kuogopa wala kusita. Taifa lazima lilindwe kwa namna yoyote," amesema.
"Ndugu zangu kwani ukitukanwa kwenye mtandao unakufa au unaumwa? Ninyi endeleeni kuelimisha hata kama watatukana matusi ya dunia nzima. Vijana ndio mna hatima ya nchi hii, msikubali kuichoma, akili za kuambiwa changanya na za kwako," amesema.
Amesema Serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo, lakini wapo watu kwa makusudi wanaaamua kubeza jitihada hizo, hivyo viongozi wa CCM wanapaswa kuwaeleza ukweli Watanzania kilichofanyika, badala ya kukaa kimya.
Vilevile, amewataka viongozi wa CCM kusimamia ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2025-2030, hasa ahadi zilizoahidiwa na Rais.
"Uchaguzi umekwisha, kazi iliyopo mbele yetu ni kwenda kukijenga Chama cha Mapinduzi, kusimamia utekelezaji wa ilani. Nendeni kuhakikisha kila jambo ambalo mgombea wetu alilinadi wakati wa kuomba kura linakwenda kukamilika," amesema na kuongeza:
"Twende tukaanze na zile siku 100 ambazo Rais Samia aliahidi, ambapo kuna ahadi alizozitoa zimeanza kutekelezwa, ikiwemo suala la ajira za afya na ualimu."
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Juma Simba ‘Gaddafi’ amesema chama hicho kimekuwa kinara wa demokrasia na kinasimamia umoja, mshikamano, upendo na kitaulinda.
"CCM tutakuwa bega kwa bega kushirikiana na Serikali maana sisi ni daraja la wananchi," amesema.
Gaddafi amesema vijana wana jukumu katika kulinda usalama wa nchi, hivyo ni muhimu kwao kushikamana nyakati zote.
Mjumbe mwingine wa halmashauri hiyo, Angellah Kairuki ameishukuru Kamati Kuu ya CCM kwa kumchagua Kihongosi, kuwa mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, akisema watampa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.