Waandishi wa Habari 40 Wapokea Mafunzo ya Mikopo ya Kilimo Mwanza
Mwanza. Zaidi ya waandishi wa habari 40 na wahariri wa Kanda ya Ziwa wamepewa mafunzo ya namna ya uendeshwaji wa mikopo inayotolewa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) mkoani Mwanza.
Warsha hiyo ya siku mbili kuanzia Desemba 3 hadi 4, 2024 pia ina lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari katika safari ya kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo nchini.
Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Alphonce Mokoki amesema vyombo vya habari vimekuwa msaada mkubwa katika kuibua fursa, kuhamasisha wakulima kutumia huduma za kifedha na kuisukuma jamii kuelekea kilimo cha kibiashara.
"Tunaendelea kuthamini mchango wenu…Kanda ya Ziwa ni kitovu kikubwa cha uzalishaji nchini, hapa ndiko kunakopatikana sehemu kubwa ya mazao ya kimkakati kama pamba, kahawa, mpunga, mahindi, mbaazi, maharage, pamoja na ufugaji wa samaki, ng’ombe na kuku," amesema.
Ameongeza kuwa, "Kwa kutambua umuhimu huu, TADB imejipanga kuhakikisha rasilimali za kifedha zinamfikia mkulima wa Kanda ya Ziwa kwa wakati na kwa ufanisi."
Ameeleza kuwa, tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2012 imetoa mikopo ya zaidi ya Sh631.18 bilioni katika miradi 151, huku Mkoa wa Mwanza ukipokea Sh79.14 bilioni katika miradi 16.
Amesema benki hiyo iliyopo chini ya Wizara ya Fedha imewezesha ufufuaji wa viwanda vinne vya kuchakata pamba (Ginneries) vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika kwa kutoa mkopo wa Sh171.58 bilioni uliotolewa hadi kufikia Oktoba, mwaka huu.
"Imewezesha upatikanaji wa masoko, kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya zao la kahawa. Bei ya kahawa maganda imeongezeka kutoka Sh1,200 hadi 5,000 kwa kilo, huku jumla ya Sh331.63 bilioni ikitolewa tayari," amesema.
Ofisa biashara wa benki hiyo, Glacia Malugujo amesema Kanda ya Ziwa ni kitovu cha ufugaji wa samaki nchini, hivyo benki hiyo imetoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba yenye thamani ya Sh12.4 bilioni kwa vikundi 120, ikihusisha wanufaika 1,904 wakiwemo vijana na wanawake.
Ameongeza kuwa wana hakikisha changamoto ya upatikanaji wa vifaranga vya sato inapungua kwa kufanya uzalishaji wa vifaranga vya kisasa kwa kutumia vitotoleshi.
Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema katika kipindi cha mwaka 2024/25, jumla ya Sh7.5 bilioni zimekopeshwa bila riba kwa vijana 350 walioko katika vikundi 47 vinavyojishughulisha na uvuvi wa kisasa wa kutumia vizimba.
Mhariri Maridhia Ngemela amesema mafunzo hayo si tu yamewaonesha fursa kama waandishi wa habari lakini pia yameongeza uelewa wao kuhusu benki hiyo ya kilimo inavyofanya kazi.