Mfamasia Momba Yasomewa Mashtaka ya Kuiba Dawa za MSD Thamani ya Sh9 Bilioni
Dar es Salaam – Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Jackson Mahagi (39) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu na kusomewa mashtaka matatu likiwemo la kuiba dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 9 mali ya Bohari ya Dawa (MSD).
Mahagi, mkazi wa Veta Manga, mkoani Mbeya, amefikishwa mahakamani Desemba 3, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 28332 ya mwaka 2025 yenye mashtaka matatu yakiwemo ya kuisababishia MSD hasara ya shilingi bilioni 9 na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka na wakili wa Serikali, Frank Rimoy, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Lyamuya alimueleza mshtakiwa kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
Vilevile, shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili mshtakiwa huyo halina dhamana, hivyo ataendelea kusalia rumande.
Mashtaka Yaliyosomewa
Katika shtaka la kwanza, wakili wa Serikali alidai kuwa kati ya Januari 2021 na Aprili 2025, Makao Makuu ya MSD yaliyopo Wilaya ya Ilala na eneo la Chitete lililopo Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Mahagi akiwa kama mtumishi na Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, aliiba dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 9.
Inadaiwa kuwa dawa hizo na vifaa hivyo vilikuwa chini yake vikitokea kwa mwajiri wake.
Shtaka la pili linadai kuwa katika tarehe hizo hizo na maeneo hayo, mshtakiwa kwa vitendo vyake hivyo aliisababishia MSD hasara ya shilingi bilioni 9.
Shtaka la tatu, Mahagi anadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha shilingi bilioni 9 huku akijua kuwa fedha hizo ni kosa tangulizi la wizi akiwa mwajiriwa.
Mchakato wa Mahakama
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama hiyo kama Mahakama ya Ukabidhi kwa ajili ya uchunguzi na maandalizi ya awali ikiwamo ukamilishaji upelelezi kabla ya kuihamishia Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza.
Hivyo kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya usikilizwaji kesi, mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake hakutakiwa kujibu lolote, mpaka kesi hiyo itakapohamishiwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya usikilizwaji kamili.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo ukaomba kesi hiyo iahirishwe mpaka tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa akisubiri kukamilika kwa upelelezi.
Mshtakiwa anatetewa na wakili Seif Wembe na amerudishwa rumande kutokana na kesi inayomkabili haina dhamana.
Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 16, 2025, itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia iwapo upelelezi umekamilika au la.