Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa amesema kundi hilo limefadhaishwa na matukio ya vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, huku wakiahidi kuendelea kuwashauri vijana watambue safari ya maendeleo yao inahitaji amani.
Ametumia jukwaa hilo kurejea historia ya kuwepo kwa kodi ya kichwa nchini, iliyochukiwa na wengi enzi hizo, akisema hakuna aliyeingia barabarani kuandamana, badala yake Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliongoza mazungumzo hadi mambo yakabadilika.
Mzee Matimbwa ameyasema hayo Jumanne Desemba 2, 2024 alipozungumza katika mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wazee wa Jiji la Dar es Salaam.
Amesema vurugu zilizotokea zimewastua na kuwafadhaisha kwa sababu zimeambatana na vifo, mali za watu zimeharibiwa na miundombinu inayosaidia watu imeathiriwa.
"Kwa kweli imetufadhaisha. Wazee tumesikitishwa na vifo vilivyotokea na uharibifu huo na tunamuomba Mungu awahifadhi wale waliotangulia na awaweke mahali pema wanapostahili," amesema.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Samia kuonyesha kuchukizwa na matukio hayo na kauli yake ya kurudisha amani.
Amesema wakati nchi inatawaliwa na wakoloni, kulikuwa na kodi ya kichwa na isingewezekana kutoka eneo moja kwenda lingine kama haujalipa.
Pamoja na yote hayo, amesema hakuna aliyeingia barabarani, bali Mwalimu Nyerere aliongoza mazungumzo na hatimaye yote yamekwisha, ndio maana kwa sasa wanashangaa yaliyotokea imekuaje.
Amesema Tanzania kitambo imekuwa kisiwa cha amani na hawana shaka chini ya uongozi wa Rais Samia hilo litadumu.
"Wazee tumefurahishwa sana na uamuzi wako wa kuanzisha wizara maalumu ya vijana ambayo ndio nguvu kazi inayotegemewa katika Taifa letu," amesema.
Amesema wataendelea kutimiza jukumu lao kama wazazi la kuwanasihi na kuwashauri katika safari yao ya maisha na kwamba ili waendelee ni muhimu amani idumishwe.
Ametumia jukwaa hilo kushukuru kwa ahadi ya kupatiwa bima ya afya ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia.
Mzee Matimbwa amependekeza kuangaliwa upya kiasi cha posho kinachotolewa kwa washauri wa mabaraza ya wazee, akisema inatolewa kiduchu hivyo vema ibadilike.
Aidha, Matimbwa amesema: "Sisi wazee wa Dar es Salaam, tunatambua kampeni zilikwenda vizuri kwa vyama vyote na michakato yote ilifanyika kwa amani na utulivu."
"Tunatambua pia upigaji kura ulikwenda vizuri hadi pale fujo na vurugu zilizopotokea, kadhia hii imetushtusha sana na kutufadhaisha kwa sababu vifo vilitokea, mali za watu na za Serikali zimeharibiwa."