Rais Samia Suluhu Hassan Atazungumza na Wazee wa Dar es Salaam Kesho
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza kwamba kesho Jumanne, Desemba 2, 2025, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atazungumza na wazee wa mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu ofisini kwake, Chalamila ameeleza kuwa mazungumzo hayo yataanza saa 5 asubuhi katika ukumbi wa mikutano ya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
"Rais Samia atatumia fursa ya mkutano na wazee hao kulihutubia Taifa," amesema Chalamila.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa Rais Samia ataambatana na viongozi wa Serikali na wasio wa Serikali ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye mazungumzo hayo kwa mustakabali wa Taifa.
"Ni mkutano mwafaka, unaorejesha matumaini na kuendelea kuponya pale ambapo Watanzania waliumia," amesema Chalamila.
Mkutano huu unatarajiwa kuwa fursa muhimu ya mawasiliano kati ya uongozi wa Taifa na wazee wa Dar es Salaam, mkoa ambao ni makao makuu ya kiuchumi ya nchi.