Serikali Yatenga Sh1 Trilioni kwa Watu Wenye Ulemavu
Dodoma. Serikali imetenga zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uchumi kupitia fursa za zabuni za umma, hatua inayolenga kuinua makundi maalumu nchini.
Kauli hiyo imetolewa Novemba 29, 2025 jijini Dodoma na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Remija Salvatory, alipozungumza na waandishi wa habari katika kongamano la watu wenye ulemavu, lililoandaliwa kuelekea siku ya kitaifa ya watu wenye ulemavu itakayofanyika mkoani Morogoro.
Salvatory amesema Serikali imeweka mkazo katika kuwathamini watu wenye ulemavu na kwa mara ya kwanza imehakikisha asilimia 30 ya zabuni za Serikali zinatengwa mahususi kwa makundi maalumu, wakiwamo watu wenye ulemavu.
"Zaidi ya Shilingi trilioni moja zimetengwa kupitia taasisi mbalimbali za Serikali, kila taasisi inalazimika kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi wa umma kwa makundi maalumu, hivyo tumekuja hapa kutoa elimu, hamasa na kuwaonyesha kwamba fursa hizi ni halali kwao," amesema.
Ameeleza kuwa hadi sasa zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh24 bilioni zimetengwa kwa ajili ya makundi hayo, ingawa idadi ya vikundi vilivyosajiliwa bado ni ndogo, vikifikia takribani 1,000 pekee nchi nzima.
"Tumehimiza watu wenye ulemavu kujiunga katika vikundi vya watu watano hadi 20 na kujisajili kwenye halmashauri zilizo karibu nao, usajili huu ndiyo utakaowatambua rasmi na kuwaruhusu kushiriki kwenye zabuni za Serikali kupitia mfumo wa NeST," amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) Mkoa wa Dodoma, Omary Luvuva, ameitaka Serikali kuimarisha utoaji wa elimu ya mikopo, ujasiriamali na mchakato wa ununuzi wa umma ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kuvuka mipaka ya fursa wanazopewa.
Luvuva amesema ingawa halmashauri zinatoa asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu, bado changamoto ya upatikanaji wake ni kubwa kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi na uelewa mdogo wa namna ya kuunda vikundi vinavyokidhi vigezo.
"Tunatamani kuona makundi haya yakivuka kiwango cha asilimia mbili na kuingia kwenye fursa kubwa kama tenda za Serikali, kwani wengi hawaombi zabuni hizi si kwa sababu hawana uwezo, bali kwa sababu hawajui taratibu na sifa zinazohitajika," amesema.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa taarifa zinazowafikia watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo kusababisha wengi kukosa fursa ambazo zimetengwa kwa ajili yao.
Luvuva ameitaka Serikali na wadau kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali, mikopo na mbinu za kufanikisha biashara ili kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu wanaoshiriki kikamilifu katika ununuzi wa umma na shughuli za kiuchumi kwa ujumla.