Ujenzi wa Madaraja Mkoani Lindi Umefikia Asilimia 88
Kilwa – Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewaagiza makandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa madaraja ya Somanga, Mtama, Kitapwa, Mikereng’ende na Matandu ambayo yaliharibiwa na mvua za El Niño mkoani Lindi, baada ya mradi kufikia asilimia 88.
Madaraja hayo, ambayo yaliharibu barabara kuu inayounganisha Dar es Salaam na mikoa ya Kusini, yaliharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana.
Akiwa kwenye ziara ya siku moja wilayani Kilwa Jumatano Novemba 26, 2025, Waziri Ulega amekagua maendeleo ya ujenzi na kuwataka makandarasi kuhakikisha madaraja hayo yanakamilika ifikapo Desemba 24, 2025, ili kurahisisha usafirishaji na mawasiliano katika mkoa huo.
"Nimeridhishwa na utendaji kazi wenu kwani hadi sasa mmebakisha asilimia chache za kumaliza ujenzi wa madaraja hayo, niwaombe kuongeza kasi ya ujenzi hadi ifikapo Desemba 24 mwaka huu miradi iwe imekamilika," amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emily Zengo, amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh119 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madaraja na makaravati yaliyoharibiwa na mvua za El Nino pamoja na kimbunga Hidaya mwaka 2024.
"Baada ya mvua kubwa kunyesha mwaka jana na kuharibu miundombinu ya madaraja Serikali ikatoa fedha zaidi ya Sh119 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya madaraja, pamoja na mikataba 13 iliyosainiwa na makandarasi wanaotekeleza ujenzi wa madaraja hayo," amesema Mhandisi Zengo.
Pia, Mhandisi Zengo amesema kwamba mradi wa ujenzi wa madaraja umeweza kuajiri vijana 200 kutoka Mkoa wa Lindi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Makapo Construction, Joseph Peneza, ameshukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa wakati na kuahidi kukamilisha ujenzi huo ifikapo Desemba 24, 2025.
"Hadi sasa daraja la Mikereng’ende limefikia asilimia 90, na pia nimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa wakati na nikuahidi Waziri ifikapo Desemba 24 mradi huu nitakuwa nimeukamilisha," amesema Peneza.