TLS Wafungua Shauri la Kikatiba Dhidi ya IGP kwa Amri ya Curfew
Dar es Salaam – Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimefungua shauri la Kikatiba dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kikipinga amri yake ya kuzuia watu kutoka nje wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Walalamikiwa wengine katika shauri hilo lililopokewa na kupewa namba 000073110 ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa vyeo vyao.
Shauri hilo lilitajwa jana Novemba 25, 2025 mbele ya jopo la majaji watatu, Immaculata Banzi, Fahamu Mtulya na Mwanabaraka Mnyukwa, ambao wameitaka TLS kuwasilisha nyaraka za madai kwa walalamikiwa kabla ya Desemba 2, 2025.
Baada ya hapo, TLS itatakiwa kuwasilisha kortini uthibitisho kuwa wamewakabidhi nyaraka hizo na walalamikiwa wamepewa siku 14 kujibu madai ya walalamikaji na wawe wamewasilisha majibu yao kortini kabla au ifikapo Desemba 16, 2025.
Shauri limepangwa kutajwa Desemba 18, 2025 kwa njia ya mtandao na wadaawa wametakiwa kuhudhuria ili siku hiyo Mahakama itoe amri kuhusu hatua inayofuata ya mchakato wa usikilizwaji wa shauri hilo.
TLS Inaomba Kuundwa Tume ya Uchunguzi
Katika shauri hilo, TLS inaiomba Mahakama itoe amri ya kuundwa tume ya watu saba ili kufanya uchunguzi huru na wa wazi kuhusu matendo yaliyotokea wakati wa zuio hilo na kuwasilisha ripoti kortini ndani ya siku 14.
Hatua ya TLS imechukuliwa wakati ambao tayari Novemba 18, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume huru kuchunguza yaliyotokea siku ya uchaguzi na siku zilizofuata, ambayo iko chini ya Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
TLS inataka tume itakayoundwa imuhusishe jaji mkuu mstaafu na wajumbe kutoka Kamisheni ya Afrika ya Haki za Watu, TLS, Chama cha Madaktari Tanzania, Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na Jumuiya ya Madola.
Ripoti hiyo kwa mujibu wa TLS, ieleze idadi na majina ya watu waliokamatwa na kuwekwa kizuizini na kiwango cha vifo vinavyotokana na kupigwa risasi moja kwa moja kwa waandamanaji, kwenye makazi ya watu na maeneo mengine ya nchi.
Vilevile, ripoti ieleze sababu nyingine za vifo vya watu ambavyo havikutokana na kupigwa risasi, sababu za majeruhi na namna risasi zilivyotumika dhidi ya waandamanaji na sababu za kukamatwa kwa maelfu ya waandamanaji.
Madai ya Ukiukwaji wa Haki za Kikatiba
TLS katika shauri hilo inataka kuwekwa taarifa ya kina ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo idadi na majina ya waliouawa, kukamatwa na kujeruhiwa na iwasilishwe mahakamani ndani ya siku 30.
Mlalamikaji anataka tume hiyo itaje watu, taasisi, mawakala na vitendeakazi, vilivyowezesha kutoa amri na kutekeleza kile alichokiita ‘kazi maalumu’ iliyofanyika kwa siku tano na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
TLS katika hati ya madai, inaeleza amri ya IGP ilikiuka Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na kwamba, zuio hilo lililodumu hadi Novemba 3, lilipoondolewa, halikuwa na uhalali kisheria na halina baraka za Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa TLS, amri hiyo ilikiuka ibara za 12(1), 13(6) (a) na (e), 14, 15(1), 17 (1), 19(1), 22(1) na 29(1) zinazohusu haki ya utu, haki ya kusikilizwa, haki ya kutotendewa unyama, haki ya kuishi, haki ya kuabudu na haki ya kufanya kazi.
Katika nyaraka zilizowasilishwa mahakamani na jopo la mawakili Jebra Kambole, Mpale Mpoki, Hekima Mwasipu na Fredrick Msaki, TLS inaeleza amri ya IGP iliyoondolewa Novemba 3, 2025 haiungwi mkono na kifungu chochote cha sheria.
Kwa mujibu wa TLS, IGP alijipa mamkala hayo wakati kulikuwa hakuna hali yoyote ya dharura, hivyo kukiuka haki zilizoainishwa Kikatiba na kwamba, amri hiyo haikusambazwa sawasawa kwa umma na ilitolewa katika kipindi kifupi mno.
"Amri iliyotolewa Oktoba 29, 2025 saa 11:00 jioni na kuondolewa Novemba 3, 2025 ilikiuka haki ya utu, haki ya kusikilizwa, haki ya kutofanyiwa unyama, haki ya kuishi, haki ya kwenda popote na haki ya kufanya kazi," inadai TLS.
Athari za Amri ya Curfew
Chama hicho kinadai amri hiyo ilitolewa saa 11:00 jioni na ikaanza kufanya kazi saa moja baadaye, saa 12:00 jioni, hivyo kukiuka haki za Kikatiba na iliathiri huduma kama upatikanaji wa bidhaa, afya, huduma za maji na nishati.
Kinadai wakati IGP anatangaza zuio na kuliondoa Novemba 3, 2025, huduma ya intaneti ilikuwa chini, hivyo iliwafikia watu wachache licha ya kwamba ilikuwa inaathiri watu wengi.
Pia, inadai wakati zuio linatolewa, halikuzingatia watu wenye ulemavu wala warahibu wa pombe, watoto na wenye matatizo ya akili na halikutolewa kwa njia ambayo lingeweza kuwafikia watu wengi jambo lililokiuka haki zao za kikatiba.
Katika shauri lililoambatanishwa kiapo cha Rais wa TLS (Boniface Mwabukusi), chama hicho kinalalamika kuwa, zuio hilo liliwaathiri pia wanachama wake na umma kwa jumla ambao walishindwa kwenda kufanya kazi na kuwanyima haki ya kuabudu.
Katika shauri hilo, TLS inaeleza wajibu wake wa msingi pamoja na mambo mengine ni kuhamasisha utawala wa sheria, uadilifu na uwazi, kusaidia umma kupata haki na kutoa misaada ya kisheria kwa umma wa Watanzania.
TLS inaeleza kuwa, IGP ambaye ndiye mjibu maombi wa kwanza, ni chombo kilichoanzishwa kisheria kwa lengo la kudumisha amani, kusimamia sheria, kuzuia na kubaini uhalifu, kukamata wahalifu na kulinda raia na mali zao.
TLS inalalamika kuwa, licha ya amri ya kutotoka nje kuwa ni haramu kisheria na iliyoelekezwa katika eneo moja la kijiografia, amri hiyo ilitekelezwa nchi nzima na mawakala wa IGP licha ya amri hiyo kuonesha ni kwa ajili ya Dar es Salaam.
Katika hati za shauri hilo, mlalamikiwa wa tatu ambaye ni Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, ana wajibu wa Kikatiba wa kuhamasisha kulindwa kwa haki za binadamu na kufanya uchunguzi wa kukiukwa kwa haki.
Siku za Giza Tanzania
TLS inadai kuwa, siku tano za zuio ambazo watazirejea kama ‘siku za giza’, kulijitokeza matukio ya kutisha ya kupigwa risasi kwa watu yaliyofanywa na wasaidizi wa mlalamikiwa wa kwanza (IGP).
"Kama chama cha mawakili, tumepokea taarifa za matukio mbalimbali ya mauaji ya watu wengi, akiwamo Wakili Peter Elibariki Makundi mwenye namba 5937 aliyeuawa na maofisa wa IGP kati ya saa 12:30 na 2:00 usiku," inaelezwa na TLS katika hati za shauri hilo.
"Kulikuwa hakuna sheria yoyote iliyompa nguvu mlalamikiwa wa kwanza kutoa amri ya aina ile ambayo imekuwa na madhara ya kukiuka haki za Kikatiba za watu."
"Amri ile haikuzingatia wafanyakazi wa sekta muhimu kama madaktari na wauguzi na pia wanaofanya kazi katika kampuni ya umeme na mawasiliano, hivyo kuuathiri umma wa Watanzania na wasio Watanzania."
"Siku hizo za giza hazikuzingatia watu wasio na makazi, watoto wa mitaani, watu wenye matatizo ya akili na makundi mengine, hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi maeneo ya Tegeta, Ubungo, Buguruni, Sinza, Mwenge na maeneo mengine," inaeleza TLS.
"Mlalamikiwa wa kwanza alitoa amri hiyo kwa kupoka mamlaka ya Rais ya kutoa amri ya dharura bila uwepo wa amri ya Mahakama au azimio la Bunge kwa hoja iliyowasilishwa na Waziri Mkuu."
Kutokana na kutokuwapo intaneti, TLS inadai ujumbe wa amri ya IGP haukusambaa kwa umma, hivyo watu walijikuta katikati ya vurugu, mashambulizi ya risasi na mauaji, huku wengine wakikamatwa na kushtakiwa kortini.