Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini washtakiwa wanne akiwemo mwandishi wa habari wa Ayo TV, Godfrey Ng’omba.
Wengine walioachiwa ni watoto watatu wa kiume wenye umri wa miaka 13, 16 na 17 ambao kwa pamoja walikuwa wakishtakiwa kwa kesi ya uhaini.
Uamuzi huo umefikiwa Jumanne Novemba 25, 2025 na Hakimu Mkazi Regina Oyier, baada ya Wakili wa Serikali kuieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Washtakiwa hao walikuwa wakishtakiwa na wenzao 59 katika kesi ya uhaini ambapo wanawakilishwa na mawakili kadhaa wakiongozwa na Khamisi Mkindi, mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Arusha.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kutenda kosa lenyewe.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29, 2025 walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.
Kosa la pili ni kufanya uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Baada ya maombi hayo, Hakimu Regina amefikia uamuzi wa kuwaachia huru bila masharti yoyote.
Jumatatu Novemba 24, 2025, washtakiwa wengine 24 wa kesi za uhaini mkoani Arusha waliachiwa na mahakama hiyo na kuwa watakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja wakitakiwa kuripoti polisi mara moja kila mwezi.