Sunday, December 7, 2025
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Idadi ya vifo katika vurugu za Oktoba 29 bado haijulikani wazi

by TNC
November 25, 2025
in Swahili
0
0
SHARES
3
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba Ajibu Maswali Kuhusu Matukio ya Oktoba 29

Dar es Salaam – Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekutana na maswali kutoka kwa wahariri kuhusu matukio ya mauaji, utekaji na idadi ya watu waliopoteza maisha Oktoba 29, maswali ambayo kwa siku kadhaa yamekuwa yakizungumzwa na wananchi na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Akiwa katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo Novemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam, Dk Mwigulu amehojiwa kuhusu kutoonekana kwa baadhi ya miili ya watu waliouawa wakati wa vurugu hizo, pamoja na sababu za Serikali kutoeleza idadi kamili ya vifo.

Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu amesema masuala ya vifo yanapaswa kushughulikiwa kwa staha, utu na huruma, si kwa mtazamo wa ushindani au sherehe. Amesisitiza kuwa kutangaza idadi ya vifo kana kwamba ni takwimu za kushabikiwa ni kuongeza majeraha kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Wito wa Kuheshimu Ubinadamu

Dk Mwiguli amekemea tabia ya kuchapisha mtandaoni taarifa au picha za vifo kwa namna inayodharirisha utu, akisema hatua hiyo haina tofauti na kusherehekea maumivu ya wengine.

Kuhusu madai ya kutotangazwa kwa idadi ya waliopoteza maisha, amesema, kama ilivyo duniani kote, vurugu huwa na madhara, na akawataka Watanzania kuepuka mijadala inayofanya maumivu ya familia kuwa mazito zaidi. Alisisitiza umuhimu wa kuweka mbele heshima kwa waliofariki na wanaoomboleza.

"Pakiwa na vurugu patakuwa na madhara na ndiyo maana wale wanaotaka kuitask (kuiwajibisha) Tanzania, kuchafua taswira yake na kufanikiwa kuwaweka Watanzania kwenye haya makovu yasiyotibika, wanatumia neno maandamano, wanaacha kuona uhalisia uliokuwepo," amesema.

Wito wa Majadiliano Badala ya Maandamano

Kuhusu swali la namna Serikali ilivyojipanga kwa maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Desemba 9, ametoa wito kwa Watanzania kurudi kwenye majadiliano ili kama kuna tatizo wakae pamoja kulitatua ili wasirudi tena nyuma katika kile kilichotokea siku ya uchaguzi.

"Ndugu zangu, hakuna vurugu yoyote iliyowahi kutokea duniani na isiwe na madhara, vurugu zikitokea expect loss of lives (tarajia vifo), expect loss of properties (tarajia uharibifu wa mali), expect divisions (tarajia migawanyiko). Haya yote yanatokea kukiwa na vurugu," amesema.

Amesisitiza kwamba kila Mtanzania awajibike kuambizana kwamba "never again" (isitokee tena), jambo kama lililotokea kwenye uchaguzi mkuu kwa sababu halina faida kwa Watanzania, lina gharama za uhai.

Waziri Mkuu amehoji kwamba wewe ungekuwa mwenye dhamana ya kulinza usalama wa watu na mali, zikatokea vurugu kama zile ungefanyaje? Ungesema acha aje…No."

Amesisitiza kwamba kuna kiapo cha kulinda nchi hii, kiapo cha kulinda mali za watu na usalama wa raia.

"Rai yetu kwa Watanzania, tusiipeleke nchi yetu kwenye jambo la aina ile ya Oktoba 29," amesisitiza Dk Nchemba ambaye ametimiza siku 12 sasa tangu alipoteuliwa na Rais Samia Novemba 13, 2025.

Dk Mwigulu amesisitiza kuwa kuna taarifa zinazowekwa mtandaoni kuhusu hekta na hekta za maeneo yaliyoathirika, lakini mitazamo inayochochea sherehe au mizaha inapotosha na kuumiza waliofikwa na misiba.

"Tuheshimu ubinadamu. Tuwape heshima familia zilizopoteza wapendwa wao, na siyo kufanya kama sherehe. Wapo wengine wanataka iwe sherehe kwa masilahi yao binafsi," amesisitiza kiongozi huyo.

Masuala ya Usalama na Utekaji

Akizungumzia madai kwamba palitolewa amri kwa polisi kuwashambulia raia katika vurugu za Oktoba 29, amesema: "Hivi pakitokea vurugu unarudi vipi nyuma kusema nishuti au nisishuti?" akibainisha kuwa maamuzi yanayochukuliwa kwenye mazingira ya hatari huwa ya papo kwa hapo ili kulinda usalama.

Kuhusu matukio ya utekaji wa watu yanayotokea nchini mara kwa mara, Dk Mwigulu amesema hilo si jambo la kutupiwa lawama vyombo vya dola, bali ni uhalifu unaopaswa kushughulikiwa kama uhalifu mwingine.

"Kuhusu watu kutekwa si jambo la kutufikisha hapa mpaka tuuane, ndiyo maana Rais ameunda Tume tupate ukweli tutoke hapa.

"Tuache kukimbilia kuamini kuwa vyombo vya dola vinahusika, nilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kilichotokea Mkuranga na Rufiji ninakijua, ulikuwa ni uhalifu," amesisitiza.

Uharibifu wa Mali – Uhujumu Uchumi

Katika mazungumzo yake, Dk Mwigulu amesisitiza kwamba uharibifu wa mali uliofanyika siku ya uchaguzi mkuu, unadhihirisha kwamba wahusika walidhamiria kuhujumu uchumi wa Tanzania kwa kuharibu miundombinu yake.

Akizungumzia uharibifu anaouhusisha na uhujumu uchumi, Dk Mwigulu amesema ofisi za Serikali 756 ambazo si nyumba za watumishi wa Serikali, zilichomwa moto wakati wa uchaguzi.

Amesema vituo vya mabasi yaendayo haraka 27, pia vilivunjwa huku mabasi sita yakichomwa moto, nyumba binafsi 273 zilichomwa moto, vituo vya polisi 159 na vituo binafsi vya mafuta 672 navyo vilichomwa moto kwenye vurugu hizo.

"Unachoma kituo cha Dawasco kinachowapa maji salama wananchi, unataka hawa watu waishije? amehoji Waziri Mkuu.

Vilevile, amesema magari ya watu binafsi 1,642 yaliteketezwa kwa moto, pikipiki binafsi 2,268 zilichomwa moto pamoja na magari ya Serikali 979.

"This is purely economic sabotage (huu hakika ni uhujumu uchumi)," amebainisha Dk Mwigulu huku akieleza kwamba waliohusika kwenye uharibifu huo ni watu wa mataifa mengine ambao wanalipwa kufanya walichokifanya.

Ameongeza kuwa: "Hii si mali ya Serikali na wala ya mtu binafsi au ya kiongozi wa Serikali, wengine walikuwa wanaongelea reli, hii si siasa hii ni mali yenu na inaghadhabisha wanaofanya hivi hawajuhi hata Kiswahili na kujifanya wanazungumza Kiswahili."

Wito wa Kulinda Tanzania

Dk Mwigulu amewataka Watanzania kuamka na kuilinda nchi yao kwa gharama yoyote ile. Amesema kuwa kuna watu wanaimezea mate Tanzania, lakini italindwa pamoja na rasilimali zake kwa gharama yoyote.

"Tanzania si nchi maskini watu wanaimezea mate, niwaambieni wale wanaomeza mate na wale wanaotumwa, niwahakikishie tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile, watameza mate mpaka yataisha.

"Tanzania hatuna rekodi ya kushindwa, tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile, kuna watu wanaimezea mate wataimezea mate mpaka yataisha," amesema Dk Mwigulu.

Amesema Watanzania wanapaswa kuamka kwani hawapendwi kiasi hicho, bali zinazotakiwa ni rasilimali zilizomo Tanzania.

"Katika maeneo mengine kuna watu wanawapa wananchi bunduki na mabomu wao wanachukua rasilimali, zilipoisha rasilimali uchonganishi na mabomu pia yakaisha," amesema.

Amesema Tanzania haitaendeshwa kwa rimoti, Mungu aliumba kila watu na nchi zao, Afrika ni ya Waafrika, Tanzania ni ya Watanzania na rasilimali zake ni za Watanzania.

Uungaji Mkono wa Tume ya Uchunguzi

Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuiunga mkono Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio ya Oktoba 29.

Amesema kumekuwa na hoja nyingi, lakini ukweli ni kuwa walioteuliwa kwenye ile tume ni wabobezi wa masuala ya namna hiyo, ambapo baadhi wamewahi kufanya hivyo katika nchi za nje na za Afrika.

Novemba 18, 2025 Rais Samia aliunda Tume Huru ya Uchunguzi kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku akimteua Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo.

Wajumbe kwenye tume hiyo ni Profesa Ibrahim Juma: Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Ombeni Sefue, Balozi Radhia Msuya, Paul Meela, Said Mwema, Balozi David Kapya na Dk Stergomena Tax.

Amesema Watanzania wamuunge mkono Rais kwa kuipa nafasi tume hiyo ifanye kazi yake.

"Niwaombe Watanzania na sisi tulichukulie jambo lililotokea kwa ukubwa wake tusiweke ajenda nyingine wala mizaha. Watu wengine tunapenda tu kujidharau kama mataifa ya Afrika na nje ya Afrika wamewaita wakatatue mambo kama haya sisi kwa nini tusiwatumie, kwani ndiyo senior citizen (watu wazima) tulionao."

"Hawa ndiyo viongozi waliobebea katika masuala haya, tuache kila mmoja kutoka na jambo lake wengi hatutajua madhara yake, hili jambo limetugharimu maisha, miundombinu na kutoaminiana," amesema Dk Mwigulu.

Mpango wa Ajira kwa Vijana

Wakati huohuo, Serikali imesema itaweka utaratibu maalumu wa kuratibu upatikanaji wa ajira kwa vijana kuanzia hatua ya matangazo hadi ajira yenyewe ili kuhakikisha usawa na kupunguza vikwazo vilivyokuwa vikikwamisha vijana kupata fursa.

Dk Mwigulu amesema kutokana na umuhimi wa vijana ndio maana Rais Samia ameunda Wizara ya Vijana itakayoshughulikia masuala yao moja kwa moja.

"Tuwe na usawa wa kijana wa Kitanzania kupata kazi kuanzia upatikanaji wa matangazo, michakato na ajira. Zamani kulikuwa na maeneo yenye wasomi wachache, lakini sasa kila mkoa una wasomi. Kupitia Wizara ya Vijana tutaratibu hili ili kuweka usawa," amesema.

Ameeleza kuwa changamoto kama tofauti za upatikanaji wa mtandao kati ya maeneo ya 2G, 3G na mijini zimekuwa zikiathiri upatikanaji wa taarifa za ajira, jambo ambalo Serikali inalenga kulitatua.

Dk Mwigulu amesema vijana hawatashinda umaskini endapo wataendelea kuamini ajira za Serikali pekee ndizo muhimu, au kudharau ajira katika sekta binafsi.

"Wasomi waliopo serikalini wakiwaona wanaofanya kazi sekta binafsi ni wa hadhi ya chini hawataushinda umaskini. Tutazungumza na kuratibu namna kijana yeyote anaweza kupata fursa ya kuajiriwa, kujiajiri au kuajiri wengine," amesema.

Ameongeza kuwa nchi haitaweza kupiga hatua iwapo vijana wataendelea kukinzana badala ya kutumia fursa zilizopo.

Tags: BadohaijulikaniIdadikatikaOktobaVifovuruguwazi
TNC

TNC

Next Post

Government turns to PPPs to tackle neonatal death rates

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company