Wapigakura Wapinga Ushindi wa Baba Levo, Wamtaja Diamond na Zuchu Mahakamani
Kigoma – Wapigakura wanne kutoka Jimbo la Kigoma Mjini wamefungua shauri mahakamani wakipinga ushindi wa Mbunge wa CCM, Clayton Chipando, maarufu kwa jina la Baba Levo.
Wapigakura hao wamewasilisha sababu 35 kuthibitisha madai yao kuwa ubunge wa Baba Levo ni batili na kuomba ufanyike uchaguzi mdogo, huku wakiwataja wasanii maarufu Diamond Platnumz na Zuchu.
Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025, Baba Levo aliyeapishwa Bungeni Novemba 11, alipata kura 35,727, akifuatiwa na Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo aliyepata kura 16,619.
Shauri hilo, lililofunguliwa Mahakama Kuu Kigoma Novemba 14, 2025, dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, Baba Levo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, linasikilizwa na Naibu Msajili Fadhili Mbelwa na litatajwa Novemba 26, 2025.
Madai ya Walalamikaji
Katika shauri namba 28949 la mwaka 2025, wapigakura hao – Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wanaiomba mahakama itamke kuwa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kigoma Mjini ni batili.
Wanaomba mahakama itamke msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na wasaidizi wake wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria kwa kuvuruga kwa makusudi mchakato wa uchaguzi.
Wanaomba kufanyika uchunguzi wa kura kuthibitisha kuwa Baba Levo hakuwa mgombea aliyepata kura nyingi, na hivyo hakustahili kutangazwa kuwa mshindi.
Aidha, wanaiomba mahakama itamuru kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo, kulipa fidia ya gharama za shauri na kugharamia mashahidi.
Sababu za Kufungua Shauri
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kortini, walalamikaji wanadai kuathiriwa kwa matokeo ya uchaguzi kutokana na kutozingatiwa kwa masharti ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024.
Ukiukaji wa Taratibu za Uchaguzi
Walalamikaji wameorodhesha vitendo 13 vinavyodaiwa kufanyika na kuathiri uhalali wa uchaguzi:
- Mawakala wa ACT Wazalendo walizuiwa kushiriki vituoni bila kuzingatia sheria
- Mawakala walinyimwa nakala za matokeo
- Kulazimishwa kusaini fomu za matokeo kabla ya kuhesabu kura
- Upigaji holela wa kura usiozingatia sheria
- Mtu mmoja kupiga kura zaidi ya moja
- Karatasi za kura kuchanwa kabla ya mpigakura kuingia kituoni
- Watu kupiga kura bila kuzingatia taarifa zao kwenye kituo
- Kufanyika kwa majumuisho ya kura bila kumjulisha mgombea wa ACT Wazalendo
- Kutobandika matokeo kwenye mbao za matangazo
- Watu kuruhusiwa kupiga kura baada ya saa 10:00 jioni
Matumizi ya Dini Katika Kampeni
Walalamikaji wanadai Baba Levo alitumia hoja za udini katika kampeni. Septemba 23, 2025, anadaiwa alitamka: "Dalali anashtaki Baba Levo anatoa rushwa anachangia madrasa, yeye ni Muislamu kwanini hachangii."
Pia anadaiwa alitumia lugha yenye lengo la kuharibu taswira ya Zitto, akimwita "Dalali" na kusema "Zitto sio Mwami tena ni Mwamini."
Septemba 9, 2025, anadaiwa alitamka: "Mimi mke wangu huyu hapa. Dalali amewahi mtambulisha mke wake? Hawezi sababu ana wanawake kila kona si watagombana."
Madai ya Rushwa
Walalamikaji wanadai Baba Levo alishiriki katika vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na:
- Septemba 25-26, 2025, kutoa Sh1 milioni kwa mwanamke aliyeitwa Mwantum kama mtaji wa biashara
- Septemba 20, 2025, kutoa Sh2 milioni kwa Kanisa la Morovian Kigoma kwa ujenzi
- Oktoba 27, 2025, Diamond Platnumz kugawia fedha wananchi wakati wa ufungaji wa kampeni
- Zuchu kutoa fedha kwa wapigakura wakati wa kampeni
Madai ya Kura Feki
Walalamikaji wanadai kuingizwa kwa kura feki na zisizo halali katika kata karibu zote, ikiwemo Machinjioni, Kasingirima, Kitongoni, Gungu, Kibirizi, Buzebazeba, Kipampa, Mwanga Kaskazini, Kagera na Ruguba.
Wanadai kwenye baadhi ya vituo, Zitto Kabwe alishinda lakini matokeo yaliebadilishwa.
Vitendo Haramu
Walalamikaji wanadai Baba Levo na watu wake walichana mabango na picha za wagombea wenzake, kufanya fujo, kupiga wapigakura na mawakala, kutoa lugha chafu na matusi, na kutishia watu na bastola.
Siku ya uchaguzi, wanamdai aliongoza operesheni ya kuteka na kukamata wapigakura na wanachama wa ACT Wazalendo kwa lengo la kuwatia hofu wasijitokeze kupiga kura.