Watu Watano Wafariki Katika Ajali ya Magari Mbuyuni, Monduli
Arusha – Watu watano wamefariki dunia na mmoja amejeruhiwa baada ya magari mawili kugongana katika maeneo ya Mbuyuni, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo leo Jumapili Novemba 23, 2025, ajali hiyo imetokea saa saba mchana katika eneo hilo.
Kupitia taarifa hiyo, Kamanda Masejo amesema ajali imehusisha magari mawili ikiwemo basi la abiria aina ya Yutong lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Arusha.
Basi hilo la abiria liligongana na gari ndogo aina ya Mark X lililokuwa likitokea Arusha na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi mmoja.
Waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume watatu na wanawake wawili, huku majeruhi akiwa ni mwanamke ambao wote walikuwa katika gari ndogo.
"Chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa na majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Jeshi Monduli kwa ajili ya matibabu, huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Makuyuni," ameeleza Kamanda Masejo kupitia taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi Arusha linatoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari na kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani wakati wote waendeshapo vyombo vya moto ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea.
Uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea ikiwa ni pamoja na utambuzi wa waliofariki.