Familia Yapata Matumaini Baada ya Nyumba Yao Kuungua Moto Mbeya
Mbeya – Familia ya watu watano walionusurika kwenye ajali ya moto na kukosa makazi wamepata matumaini baada ya Taasisi ya Tulia Trust kuanza ujenzi wa nyumba ya kisasa.
Tukio la moto lilitokea Septemba 5, mwaka huu, katika Mtaa wa Mwafute, Kata ya Ilemi kwenye nyumba ya mzee Anyomwisye Mwalyaje (80).
Ofisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust, Addi Kalinjila, amesema hatua hiyo ni sehemu ya kugusa jamii kupitia programu maalumu ya kusaidia wananchi.
"Tumekuwa na programu maalumu ya ‘Tulia Trust mtaani kwetu’ kwa kusaidia wananchi hususani ujenzi wa makazi kwa kaya maskini, wazee na yatima ambapo kwa mwaka mmoja wamezifikia kaya 22," amesema Kalinjila.
Amehamasisha jamii na viongozi wa Serikali za mitaa kutoa taarifa za watu wenye mahitaji wakiwepo wazee na kaya maskini ili waweze kuwafikia na kurejesha tabasamu hususani kuwajengea makazi bora na kutoa Bima za Afya bure.
Viongozi Washukuru Msaada
Diwani wa Kata ya Ilemi, Baraka Zambi, amesema hatua ya Taasisi hiyo ya kugusa wananchi wenye changamoto ni ya kusifiwa.
"Baada ya kutokea tukio hilo la makazi ya familia ya Kasemba Mwalyaje kuteketea kwa moto, tulitoa taarifa na ahadi ya kujenga haraka kupitia taasisi ilitekelezwa kwa vitendo," amesema Zambi.
Wakati huo huo amewataka vijana kuachana na propaganda za mtandaoni na badala yake kugeukia kuchapa kazi kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mjumbe wa nyumba kumi Mtaa wa Mwafute Kata ya Ilemi, Erasto Clement, amesema hatua ya ujenzi wa makazi ya familia hiyo inakwenda kurejesha matumaini yaliyopotea kwa kukosa makazi.
"Siku ya tukio nilikuwa mbali kidogo nilipigiwa simu kuwa nyumba ya wazee wetu inateketea kwa moto. Nilitoa taarifa kwenye mamlaka husika ambao walifika haraka kuzima licha ya mali na makazi yalikuwa tayari yameharibika," amesema Clement.
Hakuna Aliyejeruhiwa
Mmoja wa wanafamilia, Nsajingwa Mwalyaje, amesema wanashukuru Mungu kwamba hakuna mtu aliyepata madhara mbali ya uharibifu wa mali na makazi.
"Chanzo za kuzuka kwa moto ni kutokana na hitilafu ya umeme, lakini siku ya tukio ndani ya nyumba kulikuwa na watu watano wakiwepo baba, mama na wajukuu watatu. Kwa niaba ya familia tunashukuru kwa msaada wa ujenzi wa makazi mapya ya kisasa," amesema Mwalyaje.