Washtakiwa 240 Wakiwemo Niffer Wafikishwa Mahakamani Kwa Kesi ya Uhaini
Dar es Salaam. Mfanyabiashara Jenifer Jovin (26), maarufu kwa jina la Niffer, pamoja na washtakiwa wengine 239 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhaini inayotokana na maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Niffer, aliyekamatwa mapema kabla ya siku ya kupiga kura, na wenzake ambao walikamatwa siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani mahakamani Ijumaa, Novemba 7, 2025.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani saa 5:54 asubuhi wakiwa ndani ya mabasi matatu ya Jeshi la Magereza. Baadhi yao walikuwa wakitembea kwa kuchechemea kutokana na majeraha ya kipigo na mengine ya risasi, huku wengine wakidaiwa kuwa bado wanatembea na risasi mwilini.
Miongoni mwao wamo waendesha bodaboda, wanafunzi, wajasiriamali wa utingo, kondakta wa daladala, mafundi ujenzi, mawakala wa huduma za pesa kwa njia ya simu, waongoza sherehe, mafundi makenika na wapambaji kumbi za sherehe.
Pia wamo watu wenye fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwanahabari Simon Makaranga (26) mkazi wa Mbagala, walimu Lucianus Luchius (28) mkazi wa Mbweni na John Mawakili (30) mkazi wa Temboni, mhasibu Paulo Malima (28) mkazi wa Changanyikeni na mtaalamu wa maabara Benadetha Laizer (26).
Usomaji wa Mashtaka
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka ya kula njama na ya uhaini katika makundi matano tofauti mbele ya mahakimu watatu tofauti.
Mahakimu wamewaeleza washtakiwa kuwa hawatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo, bali zitasikilizwa na Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.
Pia mahakimu wamewaeleza washtakiwa kwa kuwa wanakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo halina dhamana, wataendelea kukaa mahabusu mpaka upelelezi wa kesi zao utakapokamilika.
Katika kesi zote, upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kesi ya Niffer na Wenzake
Kundi la kwanza lililomhusisha Niffer lilikuwa na jumla ya washtakiwa 22 akiwemo yeye. Katika uchunguzi wa awali (PI) namba 26388 ya mwaka 2025, Niffer na wenzake wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya.
Niffer anakabiliwa na mashtaka mawili: shtaka la kula njama kutenda kosa la uhaini linalomhusisha yeye na wenzake 21, na lingine la uhaini linalomhusu yeye peke yake. Wenzake 21 kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la uhaini linalowahusu wao pekee.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Clemence Kato, amedai washtakiwa wote kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 1 na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, amedai Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Ubungo, Dar es Salaam, washtakiwa 21 na Niffer walitengeza nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi Nyingine
Kesi ya pili ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26395 ya mwaka 2025 iliwajumuisha washtakiwa 75, ikiwa ni pamoja na Paulina Palangyo (28) mfanyabiashara mkazi wa Mbezi na wengine 74.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube, ya kula njama na uhaini yanayowahusu washtakiwa wote. Makosa hayo yanadaiwa kufanyika kati ya Aprili 1 na Oktoba 29, 2025.
Madai ya Unyanyasaji
Mawakili wanaowatetea washtakiwa wamewasilisha hoja mahakamani wakidai wateja wao waliteswa wakati wakiwa chini ya Jeshi la Polisi. Jopo la mawakili Peter Kibataka, Dickson Matata na Paul Kisabo waliwasilisha hoja hizo.
Kibatala alidai Novemba 6, 2025 Niffer akiwa chini ya Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi Oysterbay alifanyiwa vitendo vya ukatili kwa kupigwa na maofisa na kulazimishwa kusaini maelezo yake.
"Pia Novemba 5, 2025 washtakiwa 21 walipigwa na Jeshi la Polisi. Kuna washtakiwa hapa wana majeraha na vidonda mwilini, hivyo tunaomba taarifa hii iingie katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi hii," alidai Kibatala.
Ameomba mahakama itoe amri washtakiwa watakapokabidhiwa kwa Jeshi la Magereza wapatiwe matibabu ya kitabibu na ripoti yake ipelekwe mahakamani.
Uamuzi wa Mahakama
Hakimu Lyamuya ameelekeza washtakiwa wapelekwe hospitali zilizopo ndani ya Magereza na ripoti za matibabu ziwasilishwe mahakamani.
Kuhusu kuondoa shtaka la kula njama, Hakimu Lyamuya na Hakimu Beda kwa nyakati tofauti wamesema mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Lyamuya ameelekeza washtakiwa wote warudishwe rumande ya magereza hadi Novemba 11, 2025, siku ambayo upande wa mashtaka utajibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi.
Kesi ya tatu iliwahusu washtakiwa John Alexander John na wengine 12, ambao wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki. Kesi hiyo itatajwa Novemba 20, 2025.
Katika kesi ya nne, washtakiwa 28 wamesomewa mashtaka mawili ya kula njama na uhaini mbele ya Hakimu Nyaki. Wakili Dickson Matata amedai wateja wake walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya siku tano, walipigwa na kuteswa, na hawakupewa haki ya kuonana na ndugu au wakili.
Hakimu Nyaki ameelekeza gereza ambako washtakiwa watapelekwa wapatiwe matibabu na ripoti iwasilishwe mahakamani.
Katika kesi ya tano, washtakiwa 95 wamesomewa mashtaka mawili ya kula njama kutenda kosa la uhaini na la uhaini mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube. Kesi hiyo itatajwa Novemba 19, 2025.