Sunday, December 7, 2025
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Vurugu zilivyotikisa sekta ya elimu

by TNC
November 5, 2025
in Swahili
0
0
SHARES
11
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Mabadiliko ya Ratiba za Mitihani na Kufungua Vyuo Baada ya Vurugu za Uchaguzi

Dar es Salaam – Sekta ya elimu imepata mtikisiko mkubwa baada ya vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025, jambo ambalo limesababisha mabadiliko ya ratiba mbalimbali muhimu.

Miongoni mwa ratiba zilizobadilishwa ni ile ya Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) inayohusisha mtihani wa upimaji wa kidato cha pili na mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Mabadiliko hayo yamefanya mtihani wa kidato cha pili uliopaswa kufanyika kuanzia Novemba 3, 2025 kusogezwa mbele hadi Novemba 10, 2025.

Ratiba nyingine iliyosogezwa mbele ni ya mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne uliopaswa kuanza Novemba 17 ambao sasa utafanyika kuanzia Novemba 24.

Vyuo Vikuu na vya Kati Vyadhihirishwa

Mabadiliko haya hayakuathiri elimu ya sekondari pekee, bali yamegusa pia taasisi za elimu ya juu ikiwemo vyuo vikuu na vya kati ambavyo vilipaswa kufunguliwa kuanzia Novemba 1, 2025.

Tangazo lililotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limewataka wanafunzi wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali waliopaswa kuripoti vyuoni Novemba 3, 2025 wasubiri tangazo jipya.

Tangazo hilo limewahusu pia wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao walitakiwa kuripoti vyuoni kuanzia Novemba 1, 2025 kwa ajili ya kuanza masomo yao ya elimu ya juu na kati.

Mitihani ya NBAA Yasogezwa

Mabadiliko ya ratiba yameigusa pia Bodi ya Wahasibu ambapo mitihani ya NBAA ya uhasibu kwa ngazi ya utunzaji vitabu (ATEC) na CPA nayo imesogezwa mbele.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali, mitihani hiyo ilipaswa kufanyika kuanzia Novemba 4 hadi 7 mwaka huu, lakini imesogezwa mbele na sasa itafanyika kuanzia Novemba 25 hadi 28.

Maoni ya Wadau wa Elimu

Akizungumzia hali hiyo, mdau wa elimu Ochola Wayoga amesema mabadiliko hayo yanaweza yasiwe na athari kubwa endapo hali itatulia na mitihani itafanyika ndani ya muda mfupi baada ya kuhairishwa.

"Hili tulilishuhudia wakati wa janga la COVID-19 shule zilifungwa na mitihani ikasogezwa mbele, hivyo si kitu kipya sana na madhara yake kwa upande mmoja yanaweza yasiwe makubwa sana, endapo itasogezwa kwa wiki moja kama ilivyoelezwa," amesema.

Wayoga amesema katika kipindi hiki ambacho watoto wamekaa nyumbani, inawezekana wamekutana na vitendo vya ukatili na hata mimba ambazo zimepatikana kutokana na kuchangamana na watu wengi nyumbani.

Amesema katika kipindi hiki ambacho shughuli za kiuchumi zimesimama, upo uwezekano wapo watoto wakachelewa kurudi shuleni au hata kushindwa kwenda kufanya mtihani kwa kukosa mahitaji, muhimu zikiwemo fedha za usafiri.

Wayoga ameongeza kwamba upo uwezekano wa athari kubwa kujitokeza zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo wanaochangia kwenye sekta ya elimu.

"Hizi vurugu tunaweza kuzichukulia kawaida ila wenzetu wakaona kwa jicho lingine, ikionekana tumeshindwa kusimamia misingi ya utawala bora kama nchi, wadau wa maendeleo wanaweza kutuwekea vikwazo vitakavyoathiri sekta ya elimu moja kwa moja, ikizingatiwa bado tunategemea fedha za wahisani," amesema Wayoga.

Athari za Kisaikolojia

Kwa upande wake, mshauri wa masuala ya elimu Dk Wilberforce Meena amesema mabadiliko ya ratiba ya mtihani yanaweza kuwa na athari za kisaikolojia kwa walimu na wanafunzi.

"Kwa mtu aliyejiandaa kufanya mtihani siku fulani halafu muda ukasogezwa, kuna namna inaweza kuathiri ile kasi ya maandalizi na athari yake iko kisaikolojia zaidi. Hili linaweza kutokea kwa wanafunzi wenyewe au hata walimu waliowandaa, ila naamini mambo yatakaa sawa," amesema.

Dk Meena amesema mabadiliko hayo ni kipimo cha uhimilivu wa mfumo wa elimu katika kuhakikisha uko tayari kukabiliana na majanga.

Maoni ya Wazazi na Walimu

Mkazi wa Kisemvule, Engebert Mwami ambaye ni mzazi, amesema hatua hiyo ya kusogeza ratiba ya mitihani hasa kwa wanafunzi wa sekondari imefanyika kwa usahihi.

"Kiukweli hakuna mzazi ambaye angekuwa na amani mtoto wake kuwa katika chumba cha mtihani katika hali hii. Mimi mwanangu yupo kidato cha pili, kwa hiki kilichofanyika naona ni busara ya hali ya juu, usalama kwanza hayo mambo mengine yanafuata," amesema Mwami.

Kwa upande wake, Asha Sefu ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari, amesema ingawa suala la kusogeza ratiba halikutarajiwa lakini itasaidia kuondoa hofu kwa wanafunzi.

"Hatujawahi kuwa na hali hii, tuliwaandaa watoto wetu kwa ajili ya mitihani lakini tatizo kama hili limetokea. Isingekuwa busara kuendelea na ratiba maana wapo ambao wangeingia chumba cha mtihani wakiwa na hofu na wengine wasingekuja kabisa," amesema.

Asha ameongeza kwamba wiki moja inaweza kusaidia wanafunzi kukaa vizuri na walimu pamoja na wazazi wakitumia kipindi hiki kuwajenga kisaikolojia na kuwaondolea hofu ili wafanye mitihani yao kwa utulivu.

Tags: ElimuSektavuruguzilivyotikisa
TNC

TNC

Next Post

Matokeo ya Darasa la Saba 2025

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company