Dar es Salaam. Serikali imetangaza kusitisha usafiri wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam ambayo hutoa huduma kati ya Gerezani – Kimara na Gerezani – Mbagala.
Kusitishwa kwa huduma hiyo kunalenga kutoa nafasi ya kufanyika kwa tathmini ili kujua uharibifu uliofanyika wakati wa maandamano yaliyofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 jijini Dar es Salaam.
Katika maandamano hayo, waandamanaji waliharibu miundombinu hususan vituo vya mwendokasi vilivyopo barabara ya Morogoro kwa kuvunja vituo, mifumo ya ukataji tiketi na kuvichoma moto baadhi ya vituo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa tangazo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Chalamila amewataka watumiaji wa usafiri huo kutafuta njia mbadala za usafiri wakati ambao unafanyika utaratibu wa kurudisha hali kama ilivyokuwa awali.
"Tunasitisha mara moja usafiri huu ili kufanya tathmini ya kina ya uharibifu uliotokea kwani mifumo ya ukataji tiketi imeharibiwa jambo ambalo linahitaji muda ili kurudisha hali kama ilivyokuwa awali," amesema Chalamila.
Ameagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya kawaida ili yaweze kutoa huduma kwa njia ambazo zilikuwa zikitegemea mabasi ya mwendokasi.