Sunday, December 7, 2025
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Siku sita za maumivu, mashaka na wasiwasi

by TNC
November 4, 2025
in Swahili
0
0
SHARES
5
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Maumivu na Mashaka: Wakazi wa Dar es Salaam Wasimulia Siku Sita za Vurugu

Dar es Salaam – Maumivu, wasiwasi na mashaka, ndiyo uhalisia wa kile walichokipitia wakazi wa baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Dar es Salaam, katika siku sita za matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani yaliyosababisha mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Matukio hayo yaliyotokea kuanzia Jumatano, Oktoba 29, 2025, yalihusisha baadhi ya wapinzani wa Serikali, kuandamana na kuchoma moto baadhi ya miundombinu vikiwemo vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, vituo vya mabasi yaendayo haraka, vituo vya mafuta, maduka na magari.

Hatua hiyo ilisababisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Camilius Wambura, kutangaza amri ya wakazi wa Dar es Salaam kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni, huku shughuli za kijamii pia zikizuiwa kama hatua ya tahadhari dhidi ya kilichokuwa kinaendelea.

Marufuku hiyo ilisababisha kubadilika kwa mtindo wa maisha ya wananchi, wengi wakisimulia maumivu, wasiwasi na mashaka walioyapitia kwa siku sita za kukaa ndani bila kwenda popote, huku kukiwa na hali ngumu ya upatikanaji wa huduma za jamii.

Vurugu Zinavyoanza

Vurugu hizo katika Jiji la Dar es Salaam zilianzia eneo la Kibo na Ubungo Maji, muda wa upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Kundi la vijana wa rika tofauti lilishuhudiwa likiifunga Barabara ya Morogoro kwa mawe na magogo.

Polisi waliokuwepo mitaani kuimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama siku ya uchaguzi, waliwatawanya vijana hao kwa mabomu ya machozi na kundi hilo kujibu mashambulizi kwa kurusha mawe.

Wakati polisi wa kutuliza ghasia wakidhibiti eneo hilo, vurugu zilihamia eneo la Ubungo Mataa, kisha Shekilango na kusambaa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Haikuchukua muda, waandamanaji walionekana wakivamia vituo vya mabasi yaendayo haraka na kuvichoma moto, huku vingine wakiishia kuvunja mageti na vioo.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa katika vituo vya mafuta, ambapo waandamanaji walivamia baadhi ya vituo hivyo na kuvichoma moto sambamba na magari yaliyokuwepo vituoni humo.

Haukuishia hapo, baadhi ya vituo vya upigaji kura vilikumbwa na msukosuko huo, kwani waandamanaji walivichoma moto na wakati mwingine kusambaratisha vifaa vilivyotumika kuhifadhia karatasi za kura na kura zenyewe.

Mashahidi Wasimulia

Katika Barabara ya Morogoro na nyingine, ilikuwa haramu kwa mwananchi kupita na chombo cha usafiri. Kila aliyepita walipo waandamanaji, walishushwa na kushurutishwa kuungana nao. Aliyegoma, usafiri wake ulichomwa moto.

Katika Barabara ya Mandela, waandamaji walichoma moto kituo cha polisi, ofisi ya Serikali za mtaa, vituo vya mafuta. Katika barabara ya Nyerere, waliharibu vituo vya mabasi ya mwendokasi na kuchoma jengo zilizopo ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) eneo la Vingunguti.

Maandamano hayo yaliendelea hadi kwenye maduka ya baadhi ya watu maarufu. Baadhi yalivamiwa na waandamanaji kuingia ndani, kuchukua kilichokuwemo kisha kuyachoma moto.

Mmoja wa mashuhuda, Wema Masatu (si jina lake halisi), ameeleza namna walivyopata ugumu kutoka Tabata Relini hadi Mbezi, wakipita njia tofauti kabla ya kushambuliwa Kimara Temboni.

"Nilipata lifti nikiwa natoka ofisini. Kwenye gari yetu tulikuwa wanne, kila njia tuliyopita hatukufanikiwa kufika mwisho. Tulirudishwa na wasamaria wema waliotushauri tutafute njia nyingine, na tukafanikiwa kupita Bonyokwa hadi kutokea Kimara Mwisho," amesema.

Amesema njiani kote walikuta vituo vingi vya kupigia kura, baadhi ya vituo vya mafuta na magari vikiwa vimechomwa.

Marufuku ya Kutoka Nje

Ilipofika saa 10 alasiri, IGP Wambura alitangaza marufuku ya wakazi wa Dar es Salaam kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni. Pia, wale wasio na ulazima wa kutembea barabarani watulie nyumbani.

Katika taarifa yake hiyo, alisema ni askari wa jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pekee ndio wanaoruhusiwa kuwepo nyakati hizo kwa ajili ya operesheni maalumu.

Kauli hiyo ilifuatiwa na ile ya Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusiluka, aliyewataka watumishi wa umma wote kufanyia kazi nyumbani Oktoba 30, isipokuwa wale ambao kazi zao zinalazimu wawepo ofisini.

Agizo hilo liliwahusu pia wafanyakazi wa sekta binafsi, huku Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikitangaza likizo fupi kwa wanafunzi wa ngazi zote na kusogeza mbele kwa wiki moja ratiba ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na nne.

Athari kwa Uchumi na Maisha

Hali ilikuwa mbaya zaidi hasa kwa wananchi ambao kula yao ilitegemea kibarua cha siku. Wengi hawakuwa na akiba wala bakaa, huku shughuli za kuwaingizia kipato zikisimama.

Matumaini yalizidi kupotea kadiri milio ya bunduki na mabomu ya kuwatawanya wananchi ilivyoendelea kusikika, kwani ilijulikana lini maandamano yalianza, lakini haikujulikana lini yangemalizika.

Ukiacha waliokosa akiba ya fedha na bakaa ya chakula, wapo wenye fedha katika mitandao ya simu na benki, nao walijikuta wakiishi sawa na wale wasiokuwa na chochote.

Hiyo ilitokana na ukweli kwamba hakukuwa na wakala wa kutoa fedha kwa mitandao ya simu, wala tawi la benki lolote lililokuwa wazi kutoa huduma za kifedha. Kila huduma ilifungwa.

Kupanda kwa Bei

Wenye maduka na magenge waliitumia hali hiyo kama fursa, wakipandisha bei ya bidhaa hasa muhimu ikiwemo chakula.

Eneo la Ubungo, kiungo kama nyanya hakikuuzwa kwa mafungu bali moja moja kwa Sh500, huku Kinondoni nyanya moja ikiuzwa Sh1,000.

Pia nauli ya bodaboda itakushangaza. Eneo lililogharimu Sh1,000 kwa usafiri huo, gharama ilipanda hadi Sh5,000. Hiyo ilitokana na kupanda kwa bei ya mafuta kutoka takriban Sh3,500 kwa lita hadi Sh10,000.

Hata hivyo, mafuta hayo hayakuuzwa kwenye vituo rasmi bali yalikuwa yakipitishwa kwenye madumu, wengine wakiwa wameshayapima na kuyahifadhi katika chupa za lita moja moja.

Emmanuel Mathias, dereva bodaboda wa Kimara Korogwe, ameeleza: "Mafuta yaliyobaki yananiwezesha kufika kituo cha mafuta pale huduma zitakapofunguliwa. Nimeshakaa siku tatu sijafanya kazi kwa sababu sina mafuta na hali haijatulia. Nimeishiwa fedha ya matumizi sijui nifanyeje."

Changamoto za Afya na Huduma

Hali ilikuwa mbaya kwa sababu hata ungeumwa, hakukuwa na namna ya kupata huduma za matibabu, kwani si maduka ya dawa wala zahanati na vituo vya afya vilivyokuwa wazi hasa jijini Dar es Salaam.

Zilizokuwa wazi ni hospitali za wilaya za baadhi ya taasisi za umma likiwemo Jeshi la Ulinzi na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo, haikuwa rahisi kuzifikia kwa kuwa barabarani ndiko walikokuwepo waandamanaji.

Familia Zatenganishwa

Maria Deogratius (si jina lake halisi) ameeleza namna alivyolazimika kumuachisha kunyonya mtoto wake mchanga.

"Vurugu zilipoanza sikuweza kufika kwangu Mbezi Malamba Mawili. Nilihifadhiwa siku nne kwa watu, baada ya kukwama njiani nikiwa natoka kazini. Nikalazimika kumwachisha mwanangu wa mwaka mmoja kunyonya," amesema.

Natalia yeye alipotezana na baba yake kwa siku sita, tangu Oktoba 29 alipotoka kwenda kazini hadi Novemba 3.

"Tulisikia alipigwa risasi ya mguu akapelekwa hospitalini. Kuanzia hapo hatukuwahi kuwasiliana naye, simu yake ilikuwa ikiita na sasa haipatikani," amesema kwa huzuni.

Maoni ya Wataalamu

Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude, amesema hali hii imeathiri kila mmoja, kwani hakuna aliyekuwa ameandaa mazingira ya kumpunguzia athari kama hali hii ingelitokea.

"Si wafanyabiashara pekee, bali watu wengi wamepata athari kwa sababu shughuli zimesimama moja kwa moja. Hata kufanya kazi nyumbani ilikuwa ngumu kwa sababu hakuna mtandao."

Amesema hali hiyo inaweza kuwa mbaya hasa kwa wale wenye madeni, huku akiwataka wanaowadai kuwapatia kipindi cha msamaha kwani huenda wakashindwa kulipa kama walivyokubaliana awali.

"Tunahitaji kuona wadau wote wanaohusika wanakaa katika meza moja. Si wote waliopo madarakani pekee, hata wale ambao hawakushiriki katika uchaguzi huu. Tuwe na maridhiano ili tuliponye taifa na tujenge uchumi kwenda mbele, kwani taifa bado lina watu wengi ambao kesho yao ina mashaka," amesema Mkude.

Tags: mashakamaumivuSikuSitaWasiwasi
TNC

TNC

Next Post

Tanzania counting economic losses in the wake of chaos that hit key sectors

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company